Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ziara rasmi ya Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, nchini Misri imekamilika kwa mafanikio makubwa, ikilenga kuimarisha mahusiano ya kitaifa na kimataifa katika nyanja za elimu, vijana na amani.
Akiwa nchini humo, Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum alipata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali wa dini pamoja na taasisi tofauti, kwa lengo la kujadili ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii. Miongoni mwa waliokutana naye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Youth Support, Bro Saleh, taasisi inayotekeleza shughuli zake nchini Uingereza na barani Afrika kwa ujumla.
Katika muendelezo wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa JMAT alialikwa kushiriki katika hafla maalum iliyoandaliwa na Irteqa Sciences University - Misri, ambapo alipata heshima ya kuwa Mgeni Rasmi na kukabidhi vyeti kwa wahitimu mbalimbali, sambamba na kushiriki jukwaa la heshima na viongozi wengine mashuhuri wa kitaaluma na kijamii.
Aidha, Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum, akiwa ameambatana na viongozi hao, alitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri, ambapo walipokelewa na kuonana na Mheshimiwa Balozi, Meja Jenerali Richardi Mutasyona Makanzo, na kujadiliana juu ya masuala ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na zile za kimataifa.
Hatua muhimu zaidi ya ziara hiyo ni kufikiwa kwa makubaliano na kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano wa kuanzisha Chuo cha Mtandaoni (Online University). Kupitia mpango huo, JMAT kwa kushirikiana na Taasisi ya Youth Support kutoka Uingereza wataendesha programu mbalimbali za masomo zitakazolenga kuwawezesha vijana kupata ajira, kuongeza ujuzi wa kitaaluma, pamoja na kujiajiri.
Kupitia juhudi hizi, Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) inaendelea kujenga misingi imara ya ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya jamii kwa ujumla, hususan katika kuwaandaa vijana kiuchumi, kielimu na kimaadili kwa mustakabali bora wa taifa.
Your Comment